Na Ahmad Mmow-Lindi
Katika kuhakikisha wakulima waliopo wilayani Kilwa hawadhulumiwi. Mkuu wa wilaya hiyo, Christopher Ngubiagai amesema atafuatilia kwa karibu mchakato wa uuzaji na ununuzi wa mazao ya kilimo ya wakulima katika vyama vya msingi vya ushirika( AMCOS) vilivyopo wilayani humo.
Jana akizungumza na Muungwana Blog katika mamlaka ya mji mdogo wa Kilwa Masoko baada ya kukamilika zoezi la kuwalipa wakulima wa ufuta katika vijiji vya Nanjirinji na Zinga ambao walikuwa hawajalipwa kutokana na fedha zao kuibwa na viongozi na watendaji wa AMCOS, alisema kuanzia sasa atakuwa anafutilia kwakaribu zaidi mchakato wa ununuzi na uuzaji wa mazao ya kilimo kwenye AMCOS zote zilizopo wilayani Kilwa.
Ngubiagai ambaye alianza kumpongeza Rais Dkt John Magufuli kwa agizo lake kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa( TAKUKURU) kuhusu fedha za wakulima wa ufuta zilizoibwa na viongozi wa AMCOS kutoa matokeo chanya kwa kipindi kifupi alisema hatasubiri kupelekewa taarifa akiwa ofisini. Bali atafanya ziara za kushitukiza za mara kwa mara kwenye ofisi za AMCOS.
"Niaapa sitakuwa na simile wala huruma na kiongozi na mtendaji yeyote wa chama cha msingi atakayejaribu kuiba fedha za wakulima. Ili niweze kufanikiwa azima hiyo nilazima nifuatilie mwenendo wa minada yote niweze kupata taarifa muhimu. Kiasi cha mazao yaliyonunuliwa, fedha walizolipwa wakulima, idadi ya waliolipwa na taarifa nyingine muhimu," alisisitiza Ngubiagai.
Alisema amejifunza mengi kupitia zoezi linaloongozwa na kaimu mkurugenzi mkuu wa TAKUKURU, Brigedia Jenerali John Mbungo dhidi ya viongozi wa AMCOS walioiba fedha za wakulima wa ufuta. Ambao baadhi yao wameanza kurejesha nakusababisha wakulima kuanza kulipwa.
"Viongozi na watendaji wa vyama vya msingi wasio waadilifu waliingiza majina hewa na kujilipa fedha za wakulima halali. Matokeo yake wakulima waliositahili kulipwa wanakosa kulipwa. Kibaya zaidi wanaolaumiwa na hata kutukanwa ni viongozi wa serikali na serikali yenyewe," alisema Ngubiagai.
Ngubiagai aliyejinasibu kwamba mkakati wake unaanza katika ununuzi na uuzaji wa korosho kwa msimu wa 2019\2020 alisema licha ya kuwadhulumu wakulima na kuwasababishia ugumu wa maisha, lakini pia watendaji na viongozi wa AMCOS wezi wamesababisha AMCOS wanazoongoza zishindwe kupiga hatua. Badala yake zinakabiliwa na madeni.
Mkuu huyo wa wilaya ya Kilwa amewataka watumishi wa umma wenye wajibu wa kusimamia, kukusanya mapato na kudhibiti mianya ya uvujaji mapato watimize wajibu wao kikamilifu. Akiweka wazi kuwa ufuatiliaji wa karibu atakaofanya utakwenda na kufika hadi kwao.
Alionya kwamba watumishi wa umma watakao bainika kushirikiana na viongozi na watendaji waovu wa AMCOS na watakaoshindwa kusimamia kikamilifu wajibu wao watalazimika kubeba machungu ya matendo na uzembe wao. Huku akisisitiza kwamba hilo sio ombi bali agizo. Kwani hana muda wa wakuwambeleza watumishi watimize wajibu wao.
Aidha Ngubiagai katika kuhakikisha wanapatikana watendaji na viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika waaminifu amewaasa wanachama wa vyama hivyo wachague watu wenye rekodi nzuri ya tabia. Kwani kosa kubwa linalosababisha vyama kuwa na watendaji na viongozi wezi ni uzembe wa wanachama wakati wa kuchagua.
Hadi sasa katika wilaya ya Kilwa pekee takribani shilingi milioni 103 ambazo ziliibwa na baadhi ya watendaji wa vyama vya msingi vya ushirika zimerejeshwa na kuanza kulipwa baadhi ya wakulima. Ambapo wakulima wasio lipwa wanaombwa kutokuwa na hofu, kwani wote watalipwa.
Thursday, October 31, 2019
DC Ngubiagai kula sahani moja na viongozi wa AMCOS
Tags
# Top News
About Sultan Mapigo
SULTAN MAPIGO: Kuwa wa kwanza kuhabarika, Tafadhari usisahau kusubscribe kushare na kucomment
Top News
Tags:
Top News
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment