Adbox

Tuesday, October 22, 2019

DC Jokate asikitishwa na jambo hili

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Mkoani Pwani, Jokate Mwegelo amedai kusikitishwa na vitendo vya vijana wa kiume kuwapiga wapenzi wao, hali inayosababisha vidonda, maumivu na hata kuhatarisha maisha ya wenzi wao ikiwemo kukatisha uhai wao.

Mkuu huyo wa wilaya ambae pia amewahi kushiriki shindano la ulimbwende nchini Tanzania mwaka 2006, amesema anashangazwa na kukithiri kwa vitendo hivyo vya ukatili licha ya elimu inayotolewa kila siku pamoja na mazingira ya kisasa yalipo.

Kutokana na hali hiyo, DC Mwegelo amesema kuwa ilitarajiwa kuonekane kuna mabadiliko katika jamii lakini hali imeonekana kuwa tofauti.

"Nikiona vijana wa kizazi hiki wakiendeleza hulka za kupiga wenza wao mpaaka kuwasababishia vidonda na maumivu makali kuhatarisha maisha na uhai. Nasikitika sana. Ungetarajia na elimu yote inayotolewa na ‘usasa’ kungekuwa na mabadiliko. Ila bado vijana wanaendeleza tamaduni mbovu." ameandika Mwegelo kupitia akaunti yake ya Twitter.

Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya Afisa msaidizi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Ruvuma, James Paul kumuua kwa kumpiga risasi tatu kichwani mpenzi wake, Beata Kafuru kutokana na kile kinachoelezwa kuwa ni wivu wa kimapenzi.

No comments:

Post a Comment

Adbox