Adbox

Friday, October 25, 2019

Chato waomba kujengewa Chuo Kikuu

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani ameiomba Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kujenga Chuo Kikuu wilayani Chato mkoani Geita, ili Wanafunzi wanaomaliza elimu ya Sekondari wilayani humo waweze kujiunga na chuo hicho.

Dkt Kalemani ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Chato, ametoa ombi hilo wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Chuo cha VETA wilayani Chato na kuongeza kuwa, tayari wilaya hiyo imetenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu.

Akizungumzia chuo hicho cha VETA kinachojengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 10. 7, Dkt Kalemani ameomba kifundishe lugha za Kimataifa ili vijana wa Chato waweze kujifunza na kupata ujuzi wa kuwahudumia Watalii watakaotembelea Hifadhi ya Burigi Chato.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Geita, - Robert Gabriel amesema kuwa, ni muhimu wilaya ya Chato kuwa na Chuo Kikuu cha Afya kwa kuwa hospitali ya Kanda inajengwa katika wilaya hiyo.

Chuo cha VETA kinachojengwa wilayani Chato, kitakua na uwezo wa kudahili Wanafunzi 480 wa muda mrefu na 800 wa muda mfupi, na hadi sasa ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 78 na ujenzi huo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

Adbox