Adbox

Friday, October 25, 2019

Biashara kati ya Tanzania na Urusi iratibiwe - Waziri Mkuu

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameutaka ubalozi wa Tanzania nchini Urusi kuratibu mipango ya wafanyabiashara wa Urusi wanaokusudia kuja nchini kuwekeza kwa kuwaunganisha na Taasisi na Wizara husika ili waweze kuwekeza mitaji yao kwa kuzingatia maslahi ya Taifa.

Ametoa agizo hilo baada ya kugundua uwepo wa wafanyabiashara wengi wa Urusi wanakusudia kuja Tanzania kwa ajili ya kuangalia maeneo ya uwekezaji pamoja na kutafuta wafanyabiashara wa Kitanzania watakaoungana nao katika uwekezaji wanaokusudia kuufanya.

“Tayari miradi imekwishawekwa ya kuwakaribiasha wawekezaji wa Urusi kuja Tanzania kwa ushawishi wa kwangu mwenyewe pamoja na ushawishi wa wafanyabiashara wa Tanzania, hivyo nisingependa wafanyabiashara hao wasumbuliwe au kukatishwa tamaa katika kutimiza nia yao hiyo.” Waziri Mkuu alisisitiza.

Alisema Mkutano baina ya wakuu wa nchi na serikali kutoka mataifa ya Afrika na Urusi uliomalizika jana Oktoba 24, 2019 ulilenga kujenga uhusiano mzuri zaidi katika nyanja mbalimbali hususani za kiuchumi.

Akizungumza baada kumalizika mkutano huo kwenye ukumbi wa Olympic Park wa Sochi nchini Urusi, Waziri Mkuu alisema Urusi imeutumia mkutano huo kueleza bayana maeneo ambayo wako tayari kushirikiana na Afrika katika kuwekeza kwa faida ya pande zote mbili.

Waziri Mkuu aliyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja na uuzaji wa zana za kilimo kama vile matrekta, sekta ya mafuta na gesi pamoja na madini, ujenzi wa miundombinu hasa reli, masuala ya elimu hasa utoaji wa nafasi za mafunzo nchini humo.

No comments:

Post a Comment

Adbox