Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini wameaswa kuendelea kuzingatia matumizi ya takwimu rasmi katika kuelimisha umma kuhusu miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali.
Akizungumza wakati akifungua warsha kwa wahariri hao leo Jijini Dodoma, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt Albina Chuwa amesema kuwa dhamira ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ni kuendelea kuhakikisha kuwa wananchi wanapata taarifa sahihi katika nyanja mbalimbali ikiwemo katika matumizi ya takwimu zinazozalishwa hapa nchini.
“NBS iko tayari kusaidia asasi za kiraia ili kuzalisha takwimu sahihi kwa kutumia miongozo na kanuni za ukusanyaji na uchakataji wa takwimu hizo kwa maslahi ya wananchi ” Alisisitiza Dkt Chuwa.
Akifafanua Dkt. Chuwa amesema kuwa takwimu ni suala la kisayansi hivyo linahitaji utaalamu katika kukusanya, kuzichakata na kuzitoa kwa maslahi ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Aliongeza kuwa Ofisi hiyo itaendelea kuvijengea uwezo Vyombo vya Habari ili viweze kuelimisha umma kwa kutoa taarifa sahihi na kutumia takwimu rasmi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala, Fedha na Masoko wa NBS, Bw. Daniel Andrew amesema kuwa Ofisi yao inatambua umuhimu wa Vyombo vya Habari katika kuelimisha umma kuhusu masuala ya takwimu na kuchochea maendeleo.
Aliongeza kuwa warsha kwa wahariri hao inalenga pamoja na mambo mengine kuwajengea uwezo kuhusu mabadiliko ya Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015 yaliyofanyika mwaka 2018 na 2019 na faida zake katika kuchochea ukuaji wa uchumi.
Aidha, Mabadiliko hayo yamechangia baadhi ya nchi kuja kujifunza faida zinazotokana na mabadiliko hayo kwa maslahi ya wananchi.
Warsha hiyo imewashirikisha Wahariri wa Vyombo vya Habari kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini wakiwemo kutoka katika Televisheni, Radio, Magazeti na mitandao ya Kijamii.
Tuesday, September 24, 2019
Wahariri wa Habari waaswa kuzingatia matumizi ya Takwimu rasmi
Tags
# Top News
About Sultan Mapigo
SULTAN MAPIGO: Kuwa wa kwanza kuhabarika, Tafadhari usisahau kusubscribe kushare na kucomment
Top News
Tags:
Top News
Subscribe to:
Post Comments (Atom)



No comments:
Post a Comment