Adbox

Saturday, September 28, 2019

Pwani yabadili tarehe ya maonesho ya viwanda

Mkoa wa Pwani umeahirisha maonesho ya viwanda yaliyopangwa kuanza Oktoba Mosi mwaka huu ili kutoa fursa kwa wadau wengi zaidi kushiriki.

Mkuu wa Mkoa huo, Mhandisi Evarist Ndikilo amewaeleza waandishi wa habari mjini Kibaha kuwa, maonesho hayo yataanza Oktoba 17 na kumalizika Oktoba 23 mwaka huu kwenye uwanja wa CCM SabaSaba.

Awali mkoa huo ulipanga kuwa na maonesho ya viwanda kwa wiki moja sanjari na Kongamano la Fursa na Biashara na Uwekezaji Oktoba tatu.

"Tarehe kumi na tisa siku ya Jumamosi kama leo ndipo kutakuwa na kongamano la uwekezaji. Tumesukuma mbele kama wiki mbili baada ya tarehe 14 mwezi wa 10 ambapo Mwenge unazimwa Lindi na sisi kama mkoa tutashiriki kikamilifu kule tuwape nafasi wenzetu wa Lindi wafanikishe tukio hili kubwa,"amesema.

Ndikilo amesema tathmini iliyofanywa ya idadi ya washiriki wa maonesho hayo na kongamano hilo imeonesha kuwa idadi ya washiriki bado ni ndogo kulinganisha na matarajio.

"Kwenye maonyesho ya viwanda tulitarajia kupata washiriki 400 lakini mpaka tarehe ya jana 27 waliokuwa wamethibitisha ni wenye viwanda 173," amesema.

Ndikilo amesema wameshawafikia washiriki zaidi ya 400 kwenye mkoa wa Pwani na mikoa ya kanda ya mashariki ukiwemo wa Dar es Salaam, Tanga na Morogoro.

Kiongozi huyo amesema, miongoni mwa waliothibitisha kushiriki ni wenye viwanda 53, wajasiriamali 100 na wenye viwanda vidogo 20, na kwamba, idadi ya waliothibitisha kushiriki ni chini ya 50% kulinganisha na matarajio.

No comments:

Post a Comment

Adbox