Adbox

Friday, September 6, 2019

Dkt. Shein asisitiza dhamira ya Serikali katika kulipa kipaumbele suala la kufanya utafiti

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza dhamira ya Serikali katika kulipa kipaumbele suala la kufanya utafiti, kuwa inalenga kuzitafutia
majibu na ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika Wizara za Serikali.

Dk. Shein amesema hayo Ikulu mjini Zanzibar, wakati akipokea taarifa ya Utekelezaji wa Mpango kazi kwa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais kwa mwaka 2018/2019.

Alisema ni muhimu kwa Idara na taasisi zote za serikali kufanya utafiti, badala ya jukumu hilo kuiachia Idara ya Mipango, Sera na Utafiti pekee.

Alisema katika kufanikisha jambo hilo, Idara zinaweza kuwatumia wataalamu wake na pale wanapokosekana, ni vyema ikatowa mafunzo kwa wafanyakazi wenye elimu ya kutosha, ili hatimae
waweze kutumika kwa kazi hiyo, na kubainisha kuwa baadhi ya tafiti hazihitaji fedha nyingi.

Aliwataka viongozi wa Idara za Serikali kujenga mapenzi ya kufanya tafiti, sambamba na kujenga uwezo wa kitaaluma ili waweze kutekeleza shughuli hizo kwa ufanisi.

Aidha, aliitaka Wizara kupitia Idara ya Sherehe na Maadhimisho ya kitaifa kuwasilisha waraka Serikalini, ili kupata muafaka baada ya kubainika kuwepo kwa baadhi ya Wizara zilizonunua vifaa mbali mbali vya sherehe, ikiwemo mashamiana kwa lengo la kuvikodisha , jambo ambalo kimsingi linapaswa kufanywa na Idara hiyo.

Akigusia mchakato wa serikali kuihamishia mjini Dodoma Idara ya Uratibu wa shughuli za Serikali iliopo Dar es Salaam, Dk. Shein alisema eneo la ardhi la ekari 30 ililopatiwa serikali ya Zanzibar
na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ni kubwa, hivyo akasisitiza azma ya Serikali ya kuihamishia Ofisi hiyo Dodoma, mara baada ya hatua ya ujenzi kukamilika.

Alisema eneo hilo linapaswa kutumika vizuri kwa kuwepo mipango mizuri ya ujenzi , kuambatana na maelekezo ya Mainjinia, pamoja na kutoa indhari ya kuhakikisha ardhi hiyo inabaki salama.

Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa Serikali kupitia vyombo vyake vya Ulinzi na Usalama imejipanga vyema na vimekuwa vikifanya juhudi kubwa kukabiliana na uingizaji wa dawa za kulevya,hivyo
akabainisha umuhimu wa kuzifanyia kazi taarifa za uhalifu katika maeneo yote, ikiwemo baharini.

Katika hatua nyengine, Dk Shein aliwakumbusha watendaji wa Ofisi hiyo, kuwa Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais kama ilivyo Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, zinahitaji
wafanyakazi wanaoheshimika na kufanya kazi zao kwa misingi nidhamu, weledi na uwajibikaji.

No comments:

Post a Comment

Adbox