Adbox

Monday, September 30, 2019

Dk. Mahiga ataka weledi upashanaji habari

Serikali kwa kutambua umuhimu wa upatikanaji wa taarifa imesema ipo tayari kuangalia vikwazo vinavyosababisha ukosefu wa taarifa sahihi, ikiwamo sheria ili uchakataji wa habari uboreke kwa manufaa ya taifa.

Aidha imesema kwamba inatambua matatizo mengi duniani yanayosababisha uhasama yanatokana na kukosekana taarifa sahihi miongoni mwa wanadamu.

Aidha kukosekana kwa taarifa sahihi na kuwapo kwa taarifa za uongo kumesababisha kuwapo kwa vita na usumbufu mwingine ambao ungeliweza kutatuliwa kwa kuwapo kwa taarifa zilizo sahihi.

Kauli hizo zimetolewa na Waziri wa Katiba na Sheria Dk. Augustine Mahiga kwenye maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Upataji Taarifa iliyoadhimishwa mkoani Morogoro hapa nchini yakiwa na kauli mbiu “Upataji Taarifa : Asiachwe Mtu!”.

Alisema ili taifa la Tanzania lisiingie katika migogoro serikali ipo tayari kusikiliza wadau na kushirikiana nao kuweka mazingira ya upatikanaji wa taarifa kuwa bora zaidi na unaojali maslahi mapana ya nchi.

Pamoja na kuwapongeza waandazi wa hafla hiyo, UNESCO,  Dk. Mahiga pia alielezea umuhimu wa taasisi za umma na binafsi zinazohusika na upashaji habari kuifanya kazi hiyo kwa uaminifu na weledi mkubwa ili kuondoa matatizo yanayoambatana na kukosekana kwa habari.

Alisema uchakataji wa habari ni muhimu ili wananchi wote waweze kupata habari na kuzitumia kwa maendeleo yao.

Alisema suala la upatikanaji wa taarifa sahihi si wa taifa moja tu bali dunia nzima na hilo limehimizwa tangu kumalizika kwa vita ya pili ya dunia ambayo kwa namna fulani ilichochewa na kukosekana kwa habari sahihi.

Alisema pamoja na dunia mataifa kuridhia haki ya kujieleza na kupata habari, mataifa na watu wengi wamekuwa wakikosa au wakinyimwa haki ya kuhabarishwa na hivyo kuzua matatizo katika jamii husika.

Alisema ndio maana Tanzania imekuwa moja ya nchi iliyotia saini mikataba uhuru na haki ya kupata habari na kutamka wazi katika katiba yake kuhusu haki za habari.

Alisema kuna manufaa makubwa kwa watu kuwa huru katika kuhabarishana kama kuongeza uelewa wa jamii katika masuala mbalimbali yakiwemo ya afya uchumi na namna ya kuishi.

Hata hivyo alisema taarifa zinapokuwa mbaya na zisizojenga husababisha migogoro na migongano katika jamii na hivyo kuitaka jamii kuhakikisha kwamba inapata taarifa sahihi na zenye kujenga jamii husika.

No comments:

Post a Comment

Adbox