Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ramadhani Kailima, amelitaka Jeshi la Polisi mkoani Dodoma kuboresha mazingira ya huduma wanazotoa kwa wananchi.
Alisema ni wajibu wa jeshi hilo kutoa elimu kwa jamii iweze kufahamu hatua za kufuata pindi wanapotaka kuwawekea dhamana ndugu zao waliopo katika vituo vya polisi.
Kailima aliyasema hayo hayo jana alipofanya ziara ya kutembelea vituo vinne vya polisi mkoani Dodoma.
Lengo la ziara hiyo iliyoandaliwa na Kitengo cha Kushughulikia Malalamiko Ndani ya Wizara hiyo ni kuangalia utendaji kazi wa jeshi hilo juu ya huduma wanazotoa kwa wananchi.
Vituo alivyotembelea ni vile vilivyopo katika Wilaya ya Dodoma Mjini ambavyo ni Kituo Kikuu (Central), Chang’ombe, Nkuhungu na Kikosi cha Usalama Barabarani.
Katika ziara hiyo, Kailima aliambatana na Mkurugenzi wa Kitengo cha Kushughulikia Malalamiko, Kamishna wa Polisi, Albert Nyamuhanga pamoja na Maafisa wengine wa kitengo hicho.
Akiwa kwenye kituo Kikuu cha Polisi (Central), Kailima alikuta idadi kubwa ya watu waliokuwa na shida mbalimbali, alitumia fursa hiyo kuzungumza nao na kuwataka waeleze kero zao.
Baada ya kuzungumza na wananchi, Kailima aliushauri uongozi wa kituo hicho kuweka mazingira mazuri ya kutoa huduma ili kuondoa mrundikano wa wananchi nje, ndani ya kituo.
“Wekeni mazingira mazuri ya mwananchi mmoja kuhudumiwa na askari mmoja kutokana na idadi ya askari ambao watakuwa zamu ili kupunguza msongamano,” alishauri.
Aliongeza kuwa; “Toeni elimu inayohusu dhamana kwa jamii ili wananchi wajipange kabla ya kuja kituoni, unakuta watu wengi wanakuja kuwawekea dhamana ndugu zao bila kujua taratibu hivyo kusababisha wajazane kituoni bila sababu,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Dodoma, Pipi Kayumba, alisema katika utendaji kazi wake, kila siku anapita kituoni hapo ili kuonana na wananchi anaowakuta kituoni, kusikiliza shida zao.


No comments:
Post a Comment