Waziri wa Madini, Doto Biteko amewaonya wamiliki wa migodi ya tanzanite Mirerani kwa fedha kidogo wanazochangia za kodi, na kusisitiza kuwa wasipolipa kodi hiyo, rungu litakapowafikia halitowaacha salama.
Aidha, waziri huyo amebainisha kuwa mpaka sasa serikali imefuta leseni 12,000 za migodi baada ya kushindwa kulipa kodi halali ya migodi hiyo ya kila mwaka.
Biteko aliyasema hayo baada ya kupokea taarifa ya Kamati aliyounda ya kutatua mgogoro wa mipaka (mitobozano) kati ya Kampuni ya Tanzanite One inayomiki kitalu C na wachimbaji wadogo wanaochimba vitalu A,B na D.
Aliwataka wamiliki wa migodi ya tanzanite iliyopo Mirerani kulipa kodi halali ya serikali kwani rungu litakapofika halitamwacha mtu salama .
Alisema inasikitika kuona katika mgodi yote ya tanzanite katika eneo hilo la Mirerani ni Sh bilioni 2.8 tu zinalipwa hali ambayo hairidhishi ambapo alibainisha kuwa kuna uwezekano wa wamiliki wengine wa migodi hiyo kutolipa kodi halali ya serikali.
Waziri alisema kule mkoani Mara mgodi mmoja tu ndio unaweza kulipa zaidi ya Sh bilioni 4.5 kwa miezi sita achilia mbali migodi mingine.
"Nawaagiza mlipe mara moja kodi hizi kihalali kabla hatujawafutia leseni, kiasi hiki cha kodi kinachokusanywa hapa Mirerani ni aibu," alisisitiza.
Akizungumzia mapendekezo ya mipaka, alisema mapendekezo zaidi ya 15 ya ripoti ya mitobozano yatafanyiwa kazi kwani serikali ya sasa haina mzaha katika mambo ya msingi hususani migogoro ya wachimbaji madini na wawekezaji.
Waziri alisema kumekuwa na kamati nyingi ziliundwa huko nyuma zaidi ya tisajawahi kufanyiwa kazi lakini kamati hiyo mapendekezo yake hayatawekwa kabatini kwani yatafanyiwa kazi mara moja bila kuonea mtu.
"Nimepokea taarifa ya kamati hii na naenda kuifanyia kazi kisha majibu mtapewa ila nauliza kwanini hapa Mirerani mnakuwa na maneno mengi kuliko migodi mingine, kama kusema watu wanasemwa sana acheni chuki fanyeni kazi maana serikali inawapenda wachimbaji wote," alisema.
Naibu Waziri wa Madini, Stanlaus Nyongo alisema serikali inaendelea kusimamia rasilimali za taifa na alitoa rai kwa watanzania kuacha tabia ya kutorosha tanzanite na kutotoa rekodi za uuzaji na uwekaji wa rekodi zake kwa makusudi.
Monday, July 29, 2019
Waziri Biteko atoa onyo kwa wamiliki wa migodi ya tanzanite Mirerani
Tags
# Top News
About Sultan Mapigo
SULTAN MAPIGO: Kuwa wa kwanza kuhabarika, Tafadhari usisahau kusubscribe kushare na kucomment
Top News
Tags:
Top News
Subscribe to:
Post Comments (Atom)


No comments:
Post a Comment