Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole amesema hajaiona nakala ya barua ya malalamiko ya kudhalilishwa iliyowasilishwa na makatibu wakuu wawili wastaafu wa chama hicho, Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana.
Polepole Jumapili kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi kupitia mtandao wa WhatsApp kuwa hajasikia malalamiko hayo kwa kuwa kwa sasa yupo kwenye ziara vijijini.
Wakati Polepole akisema hajasikia malalamiko hayo ambayo si tu yameandikwa na vyombo vya habari, waraka wake pia umesambaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii ikiwamo WhatsApp na hivyo kuzua mjadala mkubwa kabla na baada ya baadhi ya wabunge wa chama hicho kuendelea kujitokeza kila siku kuwajibu wastaafu hao.
Polepole ambaye alitafutwa na gazeti hili kwa ajili ya kupata ufafanuzi wa CCM kuhusu barua hizo na hatua ambazo itachukua dhidi ya malalamiko ya viongozi hao wastaafu wa chama hicho, alisisitiza kuwa atakapoiona atatujuza.
Jumapili iliyopita Makamba na Kinana walimwandikia barua Katibu wa baraza la ushauri la viongozi wakuu wastaafu wa CCM, Pius Msekwa wakilalamika kudhalilishwa kwa mambo ya uzushi na uongo na mtu anayejitambulisha kama mwanaharakati na mtetezi wa serikali na kushangaa chama hicho kukaa kimya.
No comments:
Post a Comment