Viongozi wa jeshi nchini Sudani wameafikiana na muungano wa upinzani nchini humo juu ya kuundwa kwa serikali ya mpito ambayo itaandaa njia kwa kurejeshwa kwa utawala wa kiraia.
Kwa mujibu wa wasuluhishi, jeshi na upinzani wamekubali kushirikiana katika kuongoza serikali hiyo itakayodumu kwa miaka mitatu na kisha kusimamia uchaguzi huru na wa haki.
Pande hizo mbili zilishindwa kufikia muafaka hapo kabla kutokana na mvutano wa kila upande ukitaka uwe na uwakilishi mkubwa zaidi kwenye baraza litakalounda serikali hiyo.
Lakini sasa wameahidi kuunda serikali huru itakayoongozwa kitaalamu pamoja na kuchunguza ghasia za hvi karibuni zilizosababisha mamia kufariki, Umoja wa Afrika (AU) umesema.
Taarifa za makubaliano hayo zilipokelewa kwa shangwe mitaani.
Sudani imejikuta ikitumbukia katika lindi la ghasia na suitafahamu toka alipong'olewa madarakani rais Omar al-Bashir kwa mapinduzi ya kijeshi mwezi Aprili.
Mapinduzi hayo yalizaliwa baada ya maandamano makubwa ya raia dhidi ya Bashir, ambaye aliingia madarakani kwa mtutu wa bunduki mwaka 1989.
- Jeshi lashambulia waandamanaji Sudan
- Watu wanaokata tamaa hukimbilia wapi?
- Sudan: Waandamanaji wamwagiwa gesi ya kutoa machozi
Siku tatu kabla ya makubaliano hayo ya mpito, makundi makubwa ya waandamanaji wakitaka baraza la kiongozi la kijeshi kuachia ngazi na kupisha utawala wa kiraia.
Watu saba waliuawa na wengine 181 walijeruhiwa katika vurumai hizo, vyombo vya serikali viliripoti.
Mazungumzo ya safari hii yalifanyika jijini Khartoum kupitia usuluhishi ulioongozwa na Waziri Mkuu wa Ethiopia na wanachama wa AU.
Wamekubaliana nini hasa?
"Pande mbili zimekubaliana kuunda baraza huru litakalokuwa na rais wa kupokezana baina ya jeshi na raia kwa kipindi cha miaka mitatu au zaidi," msuluhishi wa AU Mohamed Hassan Lebatt amewaambia wanahabari Ijumaa asubuhi.
Uchaguzi utafanyika pale kipindi cha mpito kitakapofikia tamati.
"Pia wamekubaliana kuwa na uchunguzi wa wazi, huru na kina juu ya matukio yote ya ghasia yaliyoikumba nchi hiyo katika wiki za hii karibuni," ameongeza.
Pia wamekubaliana kuahirisha kuanzishwa kwa baraza la wawakilishi.
"Tunaamini kuwa huu ni mwanzo wa zama mpya," amesema Omar al-Degair, kiongozi wa muungano wa wapinzani nchini humo FFC.
Naibu kiongozi wa baraza la mpito la jeshi TMC, Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, amesema: "Makubaliano haya yatakuwa ni makubwa na hayatamuacha mtu yeyote.
"Tunaushukuru Umoja wa Afrika na Ethiopia kwa kutuma wasuluhishi na kuwa wavumilivu."
Matukio kabla ya makubaliano
Mwezi uliopita, wawakilishi wa waandamanaji walikuwa katika meza ya mazungumzo juu ya nani anatakiwa kuongoza Sudani.
Lakini majadiliano yakavunjika baada ya jeshi kushambulia waandamanaji Juni 3 na kuua makumi ya waandamanaji.
Jeshi likatangaza kuwa limevunja makubaliano yote na wapinzani baada ya tukio hilo, na uchaguzi ungefanyika ndani ya miezi tisa.
Lakini wanaharakati wakasisitiza kuwa serikali ya mpito ya miaka mitatu inahitajika ili kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki unafanyika.
Baada ya mazungumzo kuvunjika, Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alipaa mpaka Sudani ili kupatanisho pande hizo mbili.
Baada ya siku kadhaa za mazungumzo, mwakilishi wa Abiy bwana Mahmoud Dirir, akatangaza kuwa viongozi wa maandamano wamekubali kurudi kwenye meza ya mazungumzo na wanajeshi.
No comments:
Post a Comment