Mashirika ya ndege ya Uingereza British Airways na Lufthansa la Ujerumani yamesitisha kwa muda safari zao kwenda Cairo, Misri kutokana na wasiwasi wa kiusalama.
British Airways ndio iliyoanza kwa kusimamisha safari zake kwa siku saba, kuanzia jana Jumamosi, kutokana na tahadhari iliyotolewa na wizara ya mambo ya nje ya Uingereza kwamba upo uwezekano mkubwa wa kufanyika mashambulio ya kigaidi. Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza imetoa tahadhari kwa raia wake wanaofanya safari kwenda Misri.
Shirika hilo la ndege la Uingereza limesema limesitisha safari zake kwa muda ili kutoa nafasi ya kufanyika tathmini kutokana na wasiwasi uliopo.
Wizara ya mambo ya nje ya Uingereza imesema ndege zinazotoka Misri kwenda Uingereza zitawekewa hatua za nyongeza za kiusalama, huku ikiwataka abiria kutoa ushirikiano kwa maafisa wa usalama kwenye viwanja vya ndege.
Wakati huo huo, shirika la ndege la Ujerumani Lufthansa limesema lilisitisha safari zake za Misri kutokea Munich na Frankfurt siku ya Jumamosi ili kufuatilia hali hiyo ingawa limesema huenda likaanza tena safari zake Jumapili.
No comments:
Post a Comment