Haroun amesema kuwa Wananchi wana Matumaini makubwa na watoa huduma wa msaada wa kisheria hivyo wanatakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na uwadilifu katika kazi zao.
Hayo ameyaeleza wakati akihutubia Wananchi katika Kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Msaada wa Kisheria yaliyaofanyika leo katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul Wakili Kikwajuni Mjini Unguja.
Waziri Haroun alisema kwamba Jamii inakabiliwa na changamoto mbali mbali ambazo zinahitaji kutatuliwa kisheria hivyo wasaidizi wa Sheria wanatakiwa kutatua changamoto hizo za jamii kwa kuzingatia uwadilifu nakuacha kufikiria maslahi yao binafsi.
Alisema wasaidizi hao wa Sheria wanatakiwa kujikita zaidi katika kutoa msaada wa kisheria na si kufikiria kufanya biashara ya huduma wanazozitoa.
“Tambueni kuwa Jamii inamatumaini makubwa na nyinyi nendeni mukafanye kazi ya kuwasaidia katika changamoto ambazo zinawakabili, musifikirie kufanya biashara, toeni huduma hizo kwa uwadilifu kama inavyotakiwa” alisema Waziri Harouni.
Aliongeza kwa kufahamisha kuwa watoa huduma wa Msaada wa kisheria ni wajibu wao kutoa huduma hizo kwa kuzingatia misingi ya utawala bora.
“Kama munavyojua chini ya Uongozi wa Dk Shein utawala bora meimarika kwa kiasi kikubwa hivyo na nyinyi nendeni mukafanye kazi kwa kuzingatia maadili, uadilifu pamoja na Utawala bora” aliongeza kusema Waziri huyo.
Aidha alifahamisha kwamba Wananchi wanashindwa kupata haki zao kutokana na kuenea kwa rushwa ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa kupotea kwa haki za wananchi kwani watendaji wanaohusika huzifanya kazi zao kibiashara hali inayodumaza ustawi wa jamiii.
Katika Maelezo yake Waziri Haroun alieleza kuwa Mfumo wa usajli wa watoa huduma za msaada wa kisheria kwa njia ya kieletroniki utaweza kusaidia katika upatikanaji wa taarifa na takwimu kwa usahihi katika matukio ya udhalilishaji pamoja na madawa ya kulevya na migogoro ya ardhi ambayo yanawasumbua sana wananchi ambao hawana uwelewa juu ya sheria.
Hata hivyo Waziri huyo alitoa wito kwa Mahakama,Jeshi la Polisi,Vituo vinavyotoa huduma za kisheria na Chuo cha Mafunzo kuwa waadilifu katika kazi zao ili kuwapatia haki zao wananchi bila ya muhali na ubaguzi.
Kwa upande wake Waziri wa Katiba na Sheria Khamis Juma Mwalim alisema Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali katika kuhakikisha wananchi wanapatia msaada wa kisheria kwa changamoto ambazo zinawakabil.
Alisema moja ya jitihada hizo ni kuanzisha mfumo ambao utawawezesha watoa huduma za msaada wa kisheria Unguja na pemba kutambulikana na Sehumu walipo.
Waziri Mwalimu alifahamisha kuwa kila mwananchi anafursa sawa kwenye haki hivyo mfumo huo ni nguzo imara katika ustawi wa kupata haki zao katika kuleta maendeleo kwa wote bila ya ubaguzi.
Mapema Mkurugenzi Idara ya Msaada wa kisheria Zanzibar Hanifa Ramadhan Said alisema kesi za udhalilishaji,jinai,madawa ya kulevya hazina msaada wa kisheria jambo linalopelekea vitendo hivyo kuongezeka hivyo uwepo wa mfumo wa msaada wa kisheria utaweza kuleta mabadiliko katika upatiknaji wa haki kwa wananchi.
Alisema tokea kuanzishwa kwa idara hiyo tayari mafanikio yameanza kupatikana kutokana na kuwepo kwa mashirikiano mazuri kutoka kwa wadau pamoja na taasisi mbalimbali zinazofanya kazi za kisheria.
Hanifa alisema kazi inayofanywa na wasaidizi wa msaada wa kisheria wa kutoa huduma kwa jamii zinafanywa bila ya malipo hivyo wananchi watoe mashirikiano ya karibu na wadau wa sheria katika kupata haki zao za msingi.
Kwa upande wa Mratibu wa Mfuko unaotoa ruzuku kwa watoaji wa msaada wa sheria (LSF) Joseph Magazi aliyomba Serikali kuongeza nguvu za kutoa elimu zaidi kwa wananchi ambao hushindwa kufika kwenye vyombo vya sheria pindi wanapopta matatizo ambayo yanahitaji msaada wa sheria hasa yale ya udhalilishaji kwa watoto.
Alisema Mfuko huo hutoa ruzuku ili wananchi waweze kupatiwa msaada kwa lengo la kupata haki zao ambazo wameshindwa kuzipata kutokana na uwezo wao mdogo.
Maadhimisho ya Wiki ya Sheria ni ya kwanza kuandaliwa na Wizara ya Katiba na Sheria chini ya Idara ya Msaada wa Kisheria.


No comments:
Post a Comment