Adbox

Friday, February 28, 2020

Dhahabu yaibeba Chunya miezi 7

HALMASHAURI ya Wilaya ya Chunya imefanikiwa kukusanya kiasi cha Sh. bilioni tisa kutokana na makusanyo ya mapato ya madini ya dhahabu kwa kipindi cha miezi saba.


Hayo yalisemwa juzi na Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Maryprisca Mahundi, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio yaliyopatikana baada ya kuanzisha soko la madini wilayani humo.

Mahundi alisema tangu kuanzishwa kwa soko hilo, mwezi Mei mwaka 2019 hadi kufikia Desemba, walifanikiwa kukusanya shilingi bilioni tisa iliyopatikana kwenye biashara ya dhahabu kuanzia soko kuu na madogo waliyafungua baada ya Rais John Magufuli kuagiza wilaya hiyo kufungua soko la pamoja la kuuzia madini.

“Tumepata faida kubwa tangu kuanzishwa soko la madini wilayani hapa, mbali na kukusanya shilingi bilioni tisa, pia halmashauri imeweza kupata Sh. milioni 400, fedha ambazo tunazitumia kwenye shughuli za maendeleo ikiwamo ujenzi wa vyumba vya madarasa na ukarabati wa zahanati na vituo vya afya,” alisema Mahundi.

Aidha, Mahundi alisema makusanyo hayo ya fedha yalipatikana baada ya kamati ya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na wachimbaji wa madini kudhibiti mianya ya uuzaji holela wa madini ya dhahabu.

Alisema katika kudhibiti biashara holela, walifungua vituo vidogo sita kutoka kwenye kila eneo linalopatikana madini kufanya biashara ya uuzaji kabla ya kufika soko kuu ambavyo ni Sangambi, Makongorosi, Itewe, Igodima Itumbi na Matundasi.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya, Bosco Mwanginde, alisema biashara ya madini imekuwa chanzo kikubwa cha mapato na kwamba wanaendelea na jitihada kuhakikisha wanadhibiti biashara holela za uuzaji wa madini ili wakusanya fedha nyingi.

Alisema wanaandaa utaratibu wa kufungua soko dogo katika kila kata au kijiji kinachojihusisha na shughuli za uchimbaji wa madini ili kukusanya mapato mengi zaidi.

Naye Ofisa Madini wa wilaya hiyo, Godson Kamihanda, alisema tangu kuanzishwa kwa soko la pamoja na madini wachimbaji wamenufaika zaidi kwa sababu serikali ilitoa bei elekezi.

Alisema licha ya biashara ya madini kuwa na tija, lakini bado kuna vikwazo kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara ambao hawataki kuuza madini kwenye mfumo wa soko badala yake wanauza kwa njia za panya.

No comments:

Post a Comment

Adbox