Adbox

Thursday, December 5, 2019

Mazingira si kikwazo kwa Wawekezaji - Waziri Sima

Na Lulu Mussa

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima
amesema Serikali imefanya mapitio ya Kanuni ya Tathmini ya Athari kwa Mazingira ili kurahisha
uwekezaji nchi.

Akizungumza na Wafanyabiashara na Wawekezaji katika Mkutano  wa Mashauriano baina yao
na Serikali katika ukumbi wa Hoteli ya Glonency mkoani  Morogoro, Naibu Waziri Sima
amesema gharama za kulipia vibali zimepungua na idadi ya siku pia imepungua kutoka siku
145 mpaka siku 95 hivi sasa.

“Ndugu zangu marekebisho haya yote yanayofanywa na Serikali, yanalenga kurahisisha
mchakato wa tathmini ya Athari kwa Mazingira na kurahisisha uwekezaji hapa nchini, Mfano
awali gharama kwa vituo vya mafuta zilikuwa zaidi ya Milioni kumi na kwa sasa gharama hizi
zimepungua hadi kufikia Milioni Nne na nyingine Milioni mbili” Sima alisisitiza.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Sima, amesema Ofisi yake inaandaa Kanuni za Wataalamu
Elekezi wa Mazingira ili kurahisisha uwekezaji kwa kuwa miradi yote ni lazima ipate cheti kutoka
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC). “Tangu tumefanya mapitio ya
Kanuni zetu, malalamiko kutoka kwa wawekezaji yamepungua kwa kiasi kikubwa sana” Sima
alisisitiza.

Hata hivyo Naibu Waziri Sima amewakumbusha washiriki wa Kikao hicho kuwa Mabadiliko ya
tabianchi ni tatizo kubwa duniani, na kutoa rai kwa umma wa watanzania kupanda miti kwa
wingi kupunguza athari za mabadiliko ya Tabianchi.

Amewaagiza wawekezaji hasa wenye Viwanda kuhakikisha wanaanzisha vitalu vya miche katika maeneo yao na kusisitiza kuwa ukaguzi wa masuala ya Mazingira katika maeneo yao utaanzia hapo.

Mkutano huu wa Mashauriano baina ya Serikali, Wafanyabiashara na Wawekezaji
umelenga  kusikiliza na kutatua changamoto zao umefanyika leo  katika ukumbi wa Hoteli ya
Glonency mkoani  Morogoro na kuendelea katika Mikoa ya Pwani na Dar es Salaam. Jumla ya
Mawaziri na Manaibu Waziri 13 wanashiriki Mkutano huu.s

No comments:

Post a Comment

Adbox