Adbox

Tuesday, October 29, 2019

Watumishi waliosababishwa uwepo wa watumishi hewa wabanwa

Watumishi 1,595 waliobainika kuchezea mfumo shirikishi wa taarifa za kiutumishi na mishahara na kusababisha uwepo watumishi hewa serikalini, wamechukuliwa hatua za kinidhamu.

Aidha, uhakiki na uondoshwaji wa watumishi hewa na wale vyenye vyeti vya kughushi, umeokoa Sh 19,838,775,680 ambazo zingetumika kuwalipa watumishi hao kwa mwezi.

Hayo yamebainishwa jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika wakati wa kufungua na kuzindua Baraza Kuu la Nne la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma.

Mkuchika alisema kuondolewa kwa watumishi 19,708 kwenye mfumo shirikishi wa taasisi za kiutumishi na mishahara wenye vyeti feki na vya kughushi kutokana na uhakiki, uliofanyika kuanzia Machi 2016 hadi Oktoba 2016, kumeokoa Sh 19,838,775,680 ambazo zingelipwa kwa watumishi hao kwa mwezi.

Aidha, alisema watumishi zaidi ya 15,000 waliobainika kuwa na vyeti vya kughushi waliondolewa katika utumishi wa umma, lengo ni kuwa na watumishi waadilifu na wenye sifa stahiki katika utekeleza majukumu ya serikali.

"Ni vyema mkafahamu kuwa watumishi 1,595 waliokasimiwa madaraka ya kusimamia mfumo shirikishi wa taarifa za kiutumishi na mishahara katika wizara, idara zinazojitegemea, wakala za serikali, sekretarieti za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa ambao walibainika kuchezea mfumo huo na kusababisha kuwepo watumishi hewa walichukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu katika utumishi wa umma," alieleza.

Alisema katika kudhibiti uwepo wa watumishi hewa, mfumo shirikishi wa taarifa za kiutumishi na mishahara, umeunganishwa na mifumo mingine inatotumiwa na taasisi za serikali kama sekretarieti ya ajira, Baraza la Mitihani la Tanzania(NECTA), Baraza la Elimu ya ufundi(NACTE), Tume ya Vyuo Vikuu Tanzanaia (TCU), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na lengo ni kupunguza na kutokomeza udanganyifu wa baadhi ya watumishi na waajiri.

Kuhusu utekelezaji wa sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma, Mkuchika alisema kutofuata
miongozo hiyo, kunaathiri uwajibikaji na uwazi na kusababisha usiri usio wa lazima katika maamuzi.

Mkuchika alisema serikali imerudisha utaratibu wa kuwapandisha watumishi wake vyeo kulingana na miongozo iliyopo. Kwamba mwaka 2017 watumishi 85,000 walipandishwa vyeo na Mei, 2019 watumishi 193,166 walipandishwa.

No comments:

Post a Comment

Adbox