Adbox

Monday, October 14, 2019

Watendaji wa halmashauri zenye miradi iliyokataliwa na Mwenge wawekwa kikaongoni

Na. Ahmad Mmow, Lindi.

Rais Dkt John Magufuli amemuagiza mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) achunguze taarifa za miradi iliyotiliwa mashaka na kukataliwa kuzinduliwa, kuwekwa mawe ya msingi na kufunguliwa na Mwenge wa Uhuru katika mbio zake za mwaka 2019.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo katika uwanja wa Ilulu, manispaa ya Lindi wakati wa kilele cha mbio za Mwenge, wiki ya vijana na kumbukizi ya miaka 20 tangu kifo cha baba wa taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Rais Magufuli alitoa agizo hilo baada ya kusikiliza na kupokea risala ya utii kutoka kwa aliyekuwa kiongozi wa mbio hizo kitaifa, Mzee Mkongea Ali alisema Taasisi hiyo inatakiwa kuchambua taarifa za miradi iliyobainika kuwa nakasoro zinazotia shaka utekelezaji wake, ambayo ipo katika halmashauri 82.

Rais alimkabidhi mkurugenzi huyo makabrasha ya taarifa hizo, huku akimtaka kutosita kuwafikisha mahakamani wote watakaobaini katika uchunguzi huo kwamba wamehusika kwa njia moja ama nyingine kuhujumu miradi hiyo.

Amemtaka kutosita kumpelekea majina ya watu ambao watabainika kuhujumu miradi hiyo, hata hivyo taasisi hiyo inaweza kushindwa kuwashughulikia kwa sababu ya nafasi zao zakiutendaji na uongozi wa umma( vigogo) ili Rais Magufuli mwenyewe ashughulike nao.

Ameitaka TAKUKURU kuchunguza kwa umakini na uhakika kila ukurasa wa taarifa za miradi hiyo. '' Tunataka Tanzania inyooke, hatutaki fedha zipelekwe kutekelezea miradi ziwe zinachezewa tu,'' alisisitiza Rais Magufuli. 

Alionesha matarajio na imani kubwa kwa ofisi ya waziri mkuu na waziri mkuu mwenyewe kwamba itafuatilia kwa karibu na hatua kwa hatua uchunguzi huo. Akiweka wazi kwamba waziri mkuu Kassim Majaliwa anauwezo huo. Kwani nimfuatiliaji mzuri.

Mbali na agizo hilo namengine aliyozungumza mkuu huyo wa nchi. Lakini pia amesema serikali itaendelea kujenga makambi ya Jeshi la Kujenga Taifa(JKT) ili vijana wengi waweze kujiunga.

Alisema kupitia JKT vijana wanajifunza ukakamavu,uadilifu na moyo wakupenda nchi( uzalendo), ujuzi na stadi za kazi. Kwahiyo serikali anayoongoza itaendelea kujenga makambi kutokana na sababu hizo ambazo ndio msingi wa kuanzishwa kwa jeshi hilo.

Awali kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Mzee Mkongea Ali akisoma risala ya utii kwa Rais alisema Mwenge ulikataa kuzindua, kuweka mawe ya msingi na kufungua baadhi ya miradi iliyopo katika halmashauri 82. Kwahiyo alimkabidhi Rais taarifa za miradi hiyo ili achukue hatua.

Mkongea alisema miongoni mwa changamoto waliyokutana nayo wakiwa katika mbio hizo nikutishwa na baadhi ya viongozi na watendaji wa baadhi ya maeneo ambayo Mwenge ulipitia miradi. Hata hivyo hawakuogopa wala kukatishwa tamaa na vitisho hivyo. Bali walisonga mbele hadi kuhitimisha mbio hizo.

No comments:

Post a Comment

Adbox