Adbox

Wednesday, October 23, 2019

Washiriki wa mkutano wa SADC wavutiwa na Vivutio Hifadhi ya Arusha


Na Ferdinand Shayo,Arusha

Washiriki wa Mkutano wa  Mawaziri wa Mazingira, Maliasili na Utalii wa nchi za SADC wametembelea Hifadhi ya Taifa ya Arusha (ANAPA) wakiongozana na ujumbe wa Tanzania na kujionea vivutio mbalimbali ikiwemo makundi ya wanyamapori kama vile nyati, nyumbu, pundamilia pamoja na maporomoko ya maji.


Ziara hiyo imelenga kuhamasisha utalii katika nchi wanachama wa SADC ikiwemo Tanzania ambayo ina vivutio vingi vya utalii ambavyo ni mbuga za wanyama, hifadhi pamoja na utalii wa utamaduni.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa kikanda, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Agnes Kayole ameeleza kufurahishwa na hifadhi ya Taifa ya Arusha ambayo ipo karibu na Mjini na ina vivutio vingi ikiwemo wanyama na maporomoko ya maji  jambo ambalo linahitaji kutangazwa ili kupata watalii wengi zaidi.

Kwa upande mwingine Mkuu wa Kitengo cha Utalii kutoka Wizara ya Utalii nchini Msumbiji Bw. Nosto Mazivile amefurahishwa na vivutio hivyo vizuri na kusisitiza kuwa vikitangazwa vizuri vitasaidia  kukuza uchumi wa Tanzania na kutoa rai kwa Tanzania kuendelea na juhudi za kutunza na kuhifadhi kwa maendeleo endelevu.

Mhifadhi wa Masuala ya Utalii  na Masoko kutoka Afrika Kusini , Rollen Fovak amesema kuwa ni mara ya kwanza kutembelea hifadhi hiyo ambapo wamejionea Ngurudoto Kreta, nyani weupe maarufu kama mbega pamoja na mapromoko ya maji ya Tululusia hivyo anajukumu la kuhamasisha mataifa mengine kutembelea hifadhi.


Sekta za Mazingira, Maliasili na Utalii zinandelea na vikao vyake kwa nchi wanachama wa SADC ambavyo vimeanza tarehe 21/10/2019 na vinatarajiwa kukamilika siku ya Ijumaa tarehe 25/10/2019 Jijini Arusha.

No comments:

Post a Comment

Adbox