Adbox

Tuesday, October 22, 2019

TBS kushirikiana na SIDO kuwezesha Wajasiriamali

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limetakiwa kushirikiana na Shirika la Kuhudumia  Viwanda Vidogo (SIDO) kuwawezesha wajasiriamali kupata maeneo bora ya kuzalishia katika karakana za SIDO.

Waziri wa Nchi , Ofisi ya Waziri mkuu, Sera, Bunge, Kazi,Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista  Mhagama ametoa wito huo jana mkoani Simiyu alopotembelea banda la TBS  wakati wa kilele cha maonesho ya tatu ya mifuko ya uwezeshaji program na vikundi vya kifedha yaliyoandaliwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Mhagama alitoa wito huo kufuatia maelezo kutoka kwa afisa wa TBS Bi. Roida  Andusamile kuwa wajasiriamali wengi wanashindwa kuthibitisha ubora wa bidhaa wanazozizalisha kutokana na kutokuwa na majengo bora ya kuzalishia.

“TBS  mnapaswa kushirikiana na SIDO  ili kuwawezesha wajjasiriamali kuzalishia katika kalakana za SIDO  na hatimaye waweze kuzalisha kwa kuzingatia viwango na kuthibitisha ubora wa bidhaa hizo,” alisisitiza Mhagama.

Akizungumza na washiriki wa maonesho hayo, Mhagama ameitaka mifuko inayotoa mikopo kwa wajasiriamali kuongeza kasi ya utoaji wa mikopo hiyo ili iweze kufikia wajasiriamali wengi nchini.

Mhagama alisema utoaji huo wa mikopo uwe na riba nafuu ili wajasiriamali wengi wanufaike nayo na amelitaka Baraza la Uwezeshaji  kusimamia mifuko ya uwezeshaji kuendelea kujitambulisha na kujitangaza kwa wananchi kupitia programu mbalimbali.

Naye mtenndaji Mkuu wa  Baraza  hilo, Bi. Beng’I Issa  amewataka  wananchi wa Simiyu  kuchangamkia fursa zinazotokana na maonesho hayo kwani uwepo wa maonesho hayo utaibua chachu ya maendeleo kwa wananchi wa Simiyu.

Alisema maonesho  haya pia yanakutanisha wajasiriamali na taasisi za serikali lengo likiwa ni kuwawezesha kurasimisha biashara zao na kuhamasisha matumizi ya mifuko ya ya kijamii pamoja na  mtandao kwa wajasiriamali.

Maonesho haya yaliyoanza Oktoba 14,2019 mpaka Oktoba 20 2019  mbali na wajasiriamali yameshirikisha  taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi zipatazo 48

Katika maonesho hayo TBS ilipata fursa ya kuwatembelea wajasiriamali  wapatao 60 wanaozalisha bidhaa mbalimbali na kuwapatia utaratibu ili waweze kusajili majengo wanayozalishia , bidhaa na kuthibitisha ubora wake.

Pia wananchi waliotembelea banda la TBS walielimishwa umuhimu kwa kutumia bidhaa zilizothibitishwa ubora na  TBS  na kuangalia muda wa matumizi wa bidhaa  wanazozinunua badala ya kuangalia bei.

No comments:

Post a Comment

Adbox