Adbox

Wednesday, October 23, 2019

TAKUKURU yanusa ubadhirifu miradi ya maji Morogoro

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Morogoro imeanzisha uchunguzi baada ya kufanya ufuatiliaji wa miradi mitatu ya maji iliyopo katika wilaya za Mvomero, Gairo na Kilombero ambayo ina jumla ya thamani Sh bilioni 3.4 baada ya kubaini utekelezaji wake haukufanyika kwa ufanisi.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa, Janeth Machulya alisema hayo katika taarifa ya kazi za taasisi hiyo mkoa huo kwa kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka huu.

"Ipo baadhi ya miradi ambayo tumebaini kuwa utekelezaji wake haukufanyika kwa ufanisi na hivyo tumechukua hatua mara moja ya kuazisha uchunguzi baada ya kufanya ufuatiliaji wa miradi hiyo,"alisema Machulya.

Miradi iliyonzishiwa uchunguzi ni uliopo Kijiji cha Mvomero, Kata ya Mvomero wenye thamani ya Sh 2,627,496,506, mwingine ni katika Kijiji cha Muhatanga, Kata ya Lumemo, Tarafa ya Ifakara wilayani Kilombero wenye thamani ya Sh milioni 393, na Mradi wa Maji Kijiji cha Kilama, Kata ya Iyongwe wilayani Gairo wa Sh 388,631,604.77.

Pamoja na kazi hizo, Machulya alisema wameanza kufuatilia utekelezaji wa ukamilishaji wa vyumba vya madarasa (maboma) katika baadhi ya shule za msingi na sekondari zilizopokea fedha za serikali ili kukamilisha ujenzi wake.

Alisema katika hatua za awali za ufuatiliaji huo zimeanza kubaini kuwepo kwa upungufu. Hivyo aliwataka viongozi wote wenye dhamana ya usimamizi wa miradi ya maendeleo ya serikali wasimamie maeneo yao kuhakikisha kuwa thamani ya fedha ya serikali kwa kila mradi inafikiwa ikiwa na wananchi kushiriki kikamilifu kufuatilia miradi hiyo kwa kuwa ni yao. Licha ya hayo alisema katika kutekeleza jukumu la kuzuia vitendo vya rushwa, Takukuru ilibaini uwepo wa tabia ya baadhi ya taasisi zisizo za kiserikali (NGO's) kukwepa kulipa kodo wanazopaswa kulipa kisheria.

Ongezeko la thamani (VAT). Alisema katika ufuatiliaji huo, TAKUKURU imefanikisha kuokoa kiasi cha Sh. 32,294,680 ambazo zililipwa katika Ofisi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na adhabu ya kuchelewa kupita kutokana na huduma iliyoitoa.

Katika hatua nyingine, Takukuru Mkoa imefungua rasmi ofisi katika Wilaya ya Malinyi ili kuwafikia wananchi kwa ukaribu tofauti na awali ambako wilaya hiyo ilikuwa ikihudumiwa na Ofisi ya Takukuru Wilaya ya Ulanga.

No comments:

Post a Comment

Adbox