Adbox

Thursday, October 17, 2019

Mkuu wa majeshi atoa wito kwa wananchi washirikiane na vyombo vya ulinzi na usalama


Na Ahmad Mmow, Nanyumbu.

Mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama( CDF), Jenearali Venance  Mabeyo ametoa wito kwa wananchi, hasa wanaoishi mipakani washirikiane na vyombo vya ulinzi na usalama na mamlaka zilizopo katika maeneo yao ili kudumisha amani na utulivu uliopo nchini.

Jenerali Mabeyo ametoa wito huo wakati wa hafla ya kufungua na kukabidhi vyumba sita vya madarasa, ofisi tatu za walimu na matundu 26 ya choo katika shule ya msingi Venance Mabeyo. Hafla hiyo imefanyika leo katika kijiji cha Pachani, kata ya Michiga, wilaya ya Nanyumbu, mkoa wa Mtwara.


Mkuu huyo wa majeshi alisema kunaumuhimu mkubwa wa wananchi hasa wanaoishi mipakani kushirikiana na vyombo vya ulinzi na mamlaka zilizopo katika maeneo yao kuhusu ulinzi. Ikiwamo kutoa taarifa za wageni wanaongia katika maeneo yao.

Kamanda Mabeyo aliwaomba wananchi wajifunze faida ya amani na utulivu kupitia nchi zenye migogoro na vurugu  ambazo zinasababisha kutoa wakimbizi ambao baadhi yao wanakimbilia na kuhifadhiwa nchini.

Alibainisha kwamba nchi isiyo na amani na utulivu, wananchi wake hawawezi kufanya kazi za maendeleo na uchumi kwa ufanisi. Kwahiyo nchi za aina hiyo haziwezi kuwa na maendeleo na ukuaji imara wa uchumi.

" Wakimbizi tunaowapokea wawe ni fundisho( somo) kwetu. Toeni taarifa kwa mamlaka husika kuhusu wageni wanaoingia katika maeneo yenu, si kila mgeni ana heri na sisi. Wengine wanania ovu, kwahiyo tusiruhusu nia yao ikamilike," alisisitiza Mabeyo.

Aidha aliwataka wahitimu wa mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa watumie vizuri mafunzo na ujuzi wanaopata wakiwa mafunzoni kwa kufanya kazi halali zitakazo waingizia vipato halali badala ya kutumia njia za mkato.

Ujenzi wa shule hiyo ambayo ilikuwa inaitwa Michiga B, kabla ya kupewa jina la mkuu huyo wamajeshi( Jenerali Venance Mabeyo) ambae pia nimlezi wake, ujenzi wake unakadiriwa kugharimu takribani shilingi 68.00 milioni. Ukiwa umefikia asilimia 98, ambapo vifaa vya ujenzi huo vimetolewa na kamanda Mabeyo.

Mbali na Mabeyo, wananchi wa kijiji hicho,wahisani na wadau wengine wamaendeleo walichangia  nguvu na fedha. Wakati ujenzi huo unafanywa na vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa( JKT) kutoka Kikosi cha Jeshi namba 843 (843 KJ) kilichopo wilayani Nachingwea.

No comments:

Post a Comment

Adbox