Adbox

Sunday, October 13, 2019

CCM haiingii kwenye uchaguzi ili kushinda tu - Dkt. Bashiru Ally

Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Bashiru Ally akiendelea na ziara Mkoa wa Lindi wilayani Liwale, hapo jana alizishauri kamati za siasa za wilaya, Kata na Matawi kutoteuwa wagombea wenye kashfa za kuhujumu Ushirika na kuuza ardhi za wananchi wanyonge na wagombea wote wenye mwenendo usioaminika kwenye jamii.

Akizungumza katika mkutano huo wa ndani wa wenyeviti wa mashina, viongozi wa Chama na serikali ngazi za Mkoa, wilaya, kata na matawi, Katibu Mkuu amesema, "Tukitaka kuzuia viongozi wababaishaji, Kangomba, Obutura, wadhulumaji wa ardhi, tuwe makini kwenye uchaguzi huu, kama kuna kiongozi aliwahi kuuza ardhi kwa kuwaibia wananchi, asiteuliwe na vikao vya CCM, na kama akihonga akapitishwa, wananchi msimchgue mtu huyo na sisi tutashughulika na waliomteua".

"CCM haiingii kwenye uchaguzi ili kushinda tu na kupata viongozi, ila tunaingia kwenye uchaguzi ili tushinde na tupate viongozi bora watakao wahudumia wananchi, kwa kuwa tumeapa kuwatumikia wananchi kwa haki" Dkt Bashiru alisisitiza

Aidha Katibu Mkuu amewaasa wanaCCM watakao shindwa kwa naman yoyote kwenye kura za maoni, kutosusa na kwenda vyama vingine kwa hasira, kwa sababu awamu hii wataweka nguvu zaidi kwa mwanaCCM atakaye hama na kwenda kugombea upinzani, hivyo, watamshinda na atakufa kisiasa.

Katibu Mkuu ameshauri kwa mwanaCCM yeyote atakayeshindwa kura za maoni kwa hujuma, atulie ashirikiane na aliyeshinda, baada ya uchaguzi atasikilizwa na waliohusika na hujuma watawajibishwa kwa mujibu wa katiba na kanuni za Chama.

Wakati huo huo, amesikiliza na kutolea maelekezo kero mbalimbali za wananchi ikiwemo migogoro ya ardhi, ndoa, huduma za kijamii n.k ambapo amewaelekeza viongozi wa serikali ngazi za wilaya kuzishughulikia kwa kuwa nyingi zilitakiwa kuishia huko. Pia ametumia fursa hiyo, kusisitiza viongozi kusikiliza changamoto za watu na kuzitafutia majawabu.

Huu ni muendelezo wa utekelezaji wa maelekezo ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) kwa viongozi kuendelea kuwa karibu na wananchi, kuwasikiliza na kushughulikia changamoto zao

No comments:

Post a Comment

Adbox