Adbox

Thursday, September 5, 2019

Tuendelee kuliombea Taifa - Waziri Jafo

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo amewataka viongozi wa dini Nchini kote kuendelea kuliombea Taifa hasa wakati huu ambao miradi mikubwa ya maendeleo inatekelezwa.

Waziri Jafo ameyasema hayo wakati akifunga Mkutano wa 82 wa Chama cha Madaktari wa Kikristo Tanzania unaofanyika chini ya Taasisi ya Huduma ya Kijamii za Kikristo(CSSC) katika ukumbi wa St. Gasper Jijini Dodoma.

Waziri Jafo amesema “Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza miradi mikubwa ambayo haijawahi kutokea tangu Uhuru, kila unapopita unaona ujenzi wa miundombinu ya barabara inaendelea, halkadhalika ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), huku mradi wa ufuaji umeme wa mto Rufiji unatekelezwa hatuna budi kuendelea kumuombea Rais wetu Dkt. John Joseph Pombe Magufuli azidi kuwa na afya njema na aweze kusimamia miradi hii hadi ukamilifu wake”.

Tunashukuru Mungu leo hii Mahakamu Kuu ya Gauteng, Africa Kusini imetoa hukumu na kuamuru ndege yetu ya Air Tanzania iliyokuwa inashikiliwa nchini humo iachiwe na mlalamikaji alipe gharama za kesi hizi ni habari njema sana kwetu na haya ni matunda ya kufanya vitu kwa nia
njema na dhamira ya dhati ya kuwainua watanzania tusiache kuomba kwa ajili ya Taifa hili aliongeza Jafo.

Wakati huo huo Waziri Jafo aliziagiza Halmashauri zenye Hospitali Teule (DDH) kuhakikisha wanafanya vikao na Taasisi za kidini zenye makubaliano ya uendeshaji wa Hospital hizo.

“Hizi tabia za Halmashauri kusema hawana hela za vikao sjui viburudisho zisikwamishe ufanyikaji wa vikao, kutaneni hata saa nane mchana mpaka kumi jioni cha msingi mjadiliane changamoto zinazokabili hospitali hizo na kuzitaftia njia ya kuzitatua kwa pamoja” alisema Jafo.

Kuna changamoto ndogondogo ambazo zinaweza kutatuliwa kwa mashauriano tu lakini unapoziacha kwa muda mrefu zinakuwa tatizo kubwa, mkiwa mnakutana ni vizuri katika uboreshaji wa huduma za Afya kwenye Halmashauri husika aliongeza Jafo.

“Taasisi za Dini mnafanya kazi kubwa sana katika Sekta ya Afya na kwa muda mrefu mmekuwa mkimiliki Hospital takribani 105 na Serikali tulikuwa na Hospital 77 tu kabla hatujaanza ujenzi wa Hospital za Wilaya 67.

Mmekuwa msaada katika kuwafikia wananchi ambao Serikali ilikua bado haijajenga Hospital niwapongeze kwa kuhakikisha huduma za Afya zinapatikana karibu na wananchi na kwa haraka hakika mmewasaidia watanzania wetu kupata huduma bora za Afya na mmeboresha afya zao
Alisema Jafo.

Halkadhalika Waziri Jafo aliweka wazi mpango wa Serikali kukamilisha mchakato wa kuajiri Watumishi wa Afya takribani 400 ambao kwa kiasi flani wataenda kupunguza uhaba wa watumishi wa Afya katika Vituo vya kiutolea huduma za Afya.

No comments:

Post a Comment

Adbox