Adbox

Thursday, September 26, 2019

Serikali kuziunga mkono asasi zenye malengo ya maendeleo


Na Ezekiel Mtonyole, Dodoma

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amesema serikali  itaendelea kuziunga mkono asasi za kiraia ambazo zina lengo la kuisaidia serikali katika kuleta maendeleo na kuwasaidia wananchi katika nyanja mbalimbali kama elimu na msaada wa kisheria.

Pia  Waziri Lugola amezionya baadhi ya asasi za kiraia ambazo zimekuwa na tabia ya kuitukana Serikali pamoja na kusema kwamba hakuna jambo lolote ambalo limefanywa na Serikali hiyo.

Waziri Lugola ameyabainisha hayo leo Jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Ofisi ya Kituo cha Haki za binadamu (LHRC) Mkoani Dodoma,  ambao ulienda sambamba na sherehe ya kutimiza miaka 24, na kuanza kwa kampeni ya miaka 25 ya Kituo  hicho na uzinduzi wa tuzo ya Majimaji ambayo hutolewa kwa mtu ambaye ametoa mchango mkubwa wa kisheria katika jamii.

Serikali itaziunga mkono asasi zenye mlengo mzuri wa kuisaidia serikali, pia Waziri Lugola amesema Serikali imebaini kuna asasi zisizokuwa za kiserikali ambazo zinaitukana Serikali pamoja na kusema kwamba hakuna jambo lolote ambalo limefanywa na Serikali hiyo.

“Siku za hivi karibuni tumebaini kuwepo kwa asasi zisizo za kiserikali ambazo zinatumia mwanya wa kukosoa Serikali lakini wanaenda mbali badala ya kukosoa serikali wanaitukana Serikali na wanaenda mbali kuipotosha jamii na wengine wakisema Serikali ya awamu ya tano haijafanya kitu,"amesema.

Amesema uanaharakati wa namna hiyo hauitendei  haki Serikali ya awamu ya tano kwani Serikali ya awamu ya tano imefanya mambo mengi ya maendeleo na inaendelea kufanya, hivyo si vyema kusema kwamba Serikali haijafanya kitu.

Amesema  anatamani siku moja lianzishwe Shirika  lisilokuwa la kiserikali linalohubiri na kutetea suala la haki na wajibu kwa Watanzania

“Tumebaini kwamba inapotokea kuminywa kwa haki ndipo unapotokea mlipuko wa kuashiria kuwa kuna uvunjifu kwa haki za binadamu umetokea, ukumbuke ikitokea raia asitimize na kutekekeleza wajibu wake na penyewe patatokea mlipuko kwa kuvunja haki za binadamu,” amesema Lugola.

Kuhusu watu kutekwa na kuuwawa, Waziri Lugola amesema, aliwataka watanzania kusonga mbele na kwamba kama kuna mtu kapotea Serikali ipo, Jeshi la Polisi linafanya kazi vizuri na hilo wamelisema sana hivyo hapendi  kulirudiarudia na kusisitiza kuwa Serikali inapaswa kuheshimiwa.

Aidha amekipongeza kituo Cha sheria za haki za binadamu (LHRC)kwa kazi nzuri wanazotoa za msaada wa kisheria hapa nchini, pia amempongeza Mkurugenzi msitaafu wa kituo hicho Heren Kijo Bisimba kwa kazi nzuri aliyoifanya na kumtaka mrithi wake kuiga mazuri hayo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo cha Haki za Binadamu Nchini (LHRC) Anna Henga amesema kuzindua ofisi hiyo Dodoma ni kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano ya kuhamishia Serikali Mkoani humo.

“Tunafurahi sisi kuwa kimbilio la watu wengi wenye kuhitaji msaada kubwa tumeendelea kubadili mitazamo kwa kuheshimu misingi ya haki za binadamu na sisi ni kimbilio la wanyonge,” alisema Anna

No comments:

Post a Comment

Adbox