Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa ameelekeza Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa ichukue hatua haraka za kisheria za kuvunja mkataba na Mkandarasi wa Kampuni ya Syscon Builders Ltd mwenye kazi ya ujenzi wa Mradi wa Maji wa Narungombe wenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 310 baada ya kukuta mradi huo umekwama kwa sababu ya kukiuka masharti ya mkataba.
Maamuzi ya Prof. Mbarawa yamekuja baada ya mkandarasi huyo kukiri kulipwa fedha zaidi ya Shilingi milioni 105 sawa na asilimia 33 ya jumla ya fedha zilizopangwa kutekeleza mradi na kuzitumia kwa matumizi mengine nje ya makubaliano ya mkataba.
Profesa Mbarawa amesema mkandarasi huyo alitakiwa awe amekamilisha mradi huo tangu mwezi Februari, 2018 na licha ya kuomba muda wa nyongeza wa miezi miwili, mradi haujakamilika na bado anaomba muda mwingine wa nyongeza, wakati wananchi wa Kijiji cha Narungombe wakiendelea kuwa na tatizo la maji.
"Kimsingi mkandarasi huyu hawezi kumaliza mradi huu hata tumpe mwaka mzima, ni mbabaishaji na hata wananchi hawana tena imani nae kwa kuwa ameshatoa ahadi ya uongo kukamilisha mradi huu," amesema Prof. Mbarawa.
‘‘Nikuombe Mwenyekiti na viongozi wa Halmashauri mfuate taratibu za kisheria mvunje mkataba na huyu mkandarasi na kazi hii ifanywe na Mamlaka ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) ndani ya muda mfupi iwe imekamilika tumalize kero ya maji Narungombe’’, ameelekeza Waziri Mbarawa.
Mradi wa Maji wa Narungombe ni miongoni mwa miradi ya maji minne ambayo ilikuwa inatekelezwa na Halmashauri ya Ruangwa kupitia fedha za Serikali Kuu kwa kusanifiwa na kusimamiwa na wataalam wa Halmashauri wenyewe. Ambapo ujenzi wake ulianza mwezi Septemba, 2018 na ulitarajiwa kukamilika mwezi Septemba, 2019.
Aidha, Prof. Mbarawa amesema Serikali itatoa fedha za matengenezo ya mashine ya Mradi wa Maji wa Mihewe katika Wilaya ya Ruangwa unaotumia teknolojia ya kuchuja maji yenye chumvi (Reverse Osmosis) baada ya kuharibika kwa vichujio (membranes) na kusababisha adha ya maji kwa wananchi. Pia, itabadilisha mfumo wa uendeshaji wa mradi huo kutoka kwenye matumizi ya jenereta na kuanza kutumia nishati ya jua ili kupunguza gharama kubwa za matumizi ya mafuta.
Akizungumza na Waziri wa Maji, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ruangwa, Rashid Nakumbya amesema mradi huo ni muhimu kwa halmashauri hiyo ukizingatia kuwa wanatarajia kuanza kwa mradi wa uchimbaji wa madini ya bunyu (graphite). Vilevile, wanategemea ongezeko kubwa la watu na kufanya huduma ya uhakika ya maji kuwa ni lazima.
Friday, September 27, 2019
Home
/
Top News
/
Prof. Mbarawa aelekeza Halmashauri ya Ruangwa kuvunja Mkataba na Mkandarasi mbabaishaji
Prof. Mbarawa aelekeza Halmashauri ya Ruangwa kuvunja Mkataba na Mkandarasi mbabaishaji
Tags
# Top News
About Sultan Mapigo
SULTAN MAPIGO: Kuwa wa kwanza kuhabarika, Tafadhari usisahau kusubscribe kushare na kucomment
Top News
Tags:
Top News
Subscribe to:
Post Comments (Atom)


No comments:
Post a Comment