Lugola amesema baadhi ya watu hao ambao wana nia mbaya ya nchi, wanakaa mitandaoni kuanzia asubuhi hadi jioni wakizusha matukio hayo machafu wakiwa na lengo la kujipatia umaarufu wa kisiasa kwa kuichonganisha Serikali Rais Dkt. John Magufuli na wananchi wake, ambayo inaendelea kufanya kazi nzuri kwa kuiletea nchi maendeleo kwa kasi zaidi.Waziri Lugola ameyasema hayo katika mkutano wa hadhara alipokuwa anajibu maswali mbalimbali ya wananchi wa Mji Mdogo wa Kisorya, Kata ya Kisorya, Jimbo la Mwibara, Wilaya ya Bunda, Mkoani Mara, leo, ambapo mmoja wa wananchi hao alimuuliza Waziri huyo kuhusu Wizara yake imejipangaje kuyasambaratisha matukio ya utekaji, kupotea watu hususani tukio la kupotea kwa mwandishi wa habari.Lazima tuwe na uchungu na taifa hili, taarifa hizi zinazoripotiwa na watu kupotea ama kutekwa zipo katika makundi mawili, moja ni taarifa za uongo, za kutengeneza, wakiwa na lengo la kujipatia umaarufu wa kisiasa, wakiropoka hovyo, na miongoni mwa watu hao wanaodaiwa kutekwa ama kupotea, wengine tumewabaini wanajiteka wenyewe, wanajipoteza wenyewe, na kuna wengine wameshafikishwa mahakamani kwa kutoa taarifa za uongo kuwa wametekwa, au kupotea,” alisema Lugola na kuongeza;
“Siku hizi kupitia mitandao ya kijamii, kuna watu wanatunga matukio ya uongo, wanatengeneza matukio ya kutekwa na kupotea, ndugu zangu Watanzania, taarifa hizi zinaweza kuigawa taifa, kusababisha machafuko na kusababisha taharuki katika jamii.”
“Ndugu wananchi, pia kuna taarifa za upotoshaji kwa watu wanaodaiwa kupotea au kutekwa kweli, lakini wengine wanasambaza taarifa za uongo, tumekuwa tukishuhudia katika baadhi ya migodi ya madini, wakitatafuta utajiri, lakini majumbani kwao walishafanya mpaka matanga wakiamini ndugu yao alishafiriki kwa kutekwa au kupotea, kumbe anatafuta utajiri machimboni,” alisema Lugola.
Alisema Serikali yoyote duniani ambayo imechukua dhamana ya kuwalinda wananchi wake halafu Serikali hiyo hiyo igeuke kuwateka na kuwaua, Serikali ya namna hiyo haipo duniani.
“Naelekeza Jeshi la Polisi, kwa wale ambao wanatunga maneno ya uongo na kuchonganisha Serikali na wananchi, muwasake popote walipo, muwakamate na muwafikishe katika vyombo vya sheria,” alisema Lugola.

No comments:
Post a Comment