Adbox

Wednesday, July 17, 2019

Polisi kushughulikia vyama vya siasa vitakavyoshawishi wananchi kuharibu uchaguzi

Waziri  wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amesema Jeshi la Polisi litahakikisha linawashughulikia wanasiasa watakaojaribu kuwashawishi wananchi kufanya fujo kwa lengo la kuvuruga uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Lugola alisisitiza kuwa, kisitokee chama chochote cha siasa kitakachojaribu kuvuruga uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika mwezi oktoba mwaka huu 2019, ambao Watanzania wengi wamejipanga kufanya uchaguzi huo kwa amani na utulivu.

Lugola ameyasema hayo katika mkutano wa hadhara alipokuwa anazungumza na wananchi wa Mji wa Kibara, Jimbo la Mwibara, Wilaya ya Bunda, Mkoani Mara, leo, ambapo amesema wananchi wajiepushe kudanganywa au kutumbukia katika mtego wowote wa wanasiasa.

“Wizara yangu kupitia Jeshi la Polisi haita kuwa tayari kuona na kumuacha raia wa Tanzania au asiye raia akijihusisha na vitendo vya kuhujumu uchaguzi au kuleta fujo, atadhibitiwa bila kujali nafasi yake, au uwezo wake kiuchumi, hii Serikali siyo ya kuchezewa, hivyo natuma salamu kama mlikuwa na mawazo hayo yaondoeni, hatutamuonea mtu huruma ambaye analengo la kuvuruga amani yetu,” alisema Lugola.

Pia Waziri Lugola alivitaka vyama hivyo viwe na uzalendo na nchi yao na pia viwe na hitikadi na malengo ya kisiasa ambayo hayaleti fujo kwa kufuata sheria za nchi.

No comments:

Post a Comment

Adbox