Adbox

Friday, August 2, 2019

Makamu wa Rais atahadharisha uharibifu mazingira



Makamu wa Rais, Samia Hassan, amesema kuna mzigo mkubwa wa kutunza mazingira katika mradi mkubwa wa uzalishaji umeme Rufiji ili kuhakikisha maji yanatiririka na hayazuiliki kwa shughuli yoyote.

Kauli hiyo aliitoa  alipokuwa akifungua Jukwaa la maendeleo endelevu kuhusu usimamizi bora wa misitu kwa upatikanaji wa rasilimali maji endelevu lililoandaliwa na Taasisi ya Uongozi.

Alisema ni lazima kujipanga vizuri ili maji yaweze kutiririka kuanzia vyanzo vya juu vya eneo hilo na yasizuilike popote.

"Sote tunajua mabwawa ya maji makubwa yanayozalisha umeme ni kwa maendeleo yetu, na tunajua mradi mkubwa wa uzalishaji umeme Rufiji utategemea mtiririko endelevu wa maji kutoka vyanzo vikuu ikiwamo mito na madakio ambayo yanaanzia kwenye misitu na maeneo mengine," alisema.

Alibainisha kuwa mwaka juzi alikuwa na kampeni ya utiririshaji maji katika mto Ruaha kutokana na hali yake kuwa mbaya kwa kipindi hicho.

"Tulienda kuangalia upande wa mbuga ya Ruaha hali ni mbaya mno nilikuta kitu ambacho sijawahi kuona duniani, sijawahi kuona kama wanyama wanaweza kupanga foleni kunywa maji na wanamtegemea tembo ambaye anachimba shimo ndio wanakunywa machozi yalinitoka,"alisema.

Alisema baada ya kuona hali hiyo alilazimika kuandaa kampeni maalum kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali ikiwamo Shirika la Wanyapori (WWF) na ndani ya miezi sita hali ilirejea kuwa nzuri kwenye mto huo.

"Nilikuta hali nzuri viboko wanaogelea, sasa ni kule juu kunakotegemea kumimina maji kwenye mradi wa matrilioni tunaotekeleza sasa Rufiji una mchango mkubwa wa kutiririsha maji," alisema.

Samia alisema wakati fedha nyingi zinatumbukizwa kwenye mradi huo wajue kuna mzigo mkubwa wa kutunza mazingira kuanzia vyanzo vya juu ili viweze kutiririsha maji na yasizuilike popote.

No comments:

Post a Comment

Adbox