Adbox

Tuesday, October 22, 2019

Watumishi TAMISEMI waaswa kuzingatia miiko ya kazi

Watumishi wa Ofisi ya Rais TAMISEMI wameaswa kutatua changamoto za watanzania kwa kuimarisha mifumo ya utendaji kazi na malalamiko ya wananchi ili kuleta maendeleo bora kwa taifa.

Hayo yamebainisdhwa leo na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Elimu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Gerald Mweli alipowasili katika ofisi za TAMISEMI zilizoko Jijini Dodoma baaada ya kupokelewa na watumishi wa wizara hiyo.

Naibu Katibu Mkuu Gerald Mweli amesema kuwa ili kufikia matokeo bora ya kuwatumikia watanzania kuna haja ya kuimarisha ushirikiano mzuri katika utendaji na watanzania wanaowahudumia kwani ndio dhima kubwa waliyonayo katika nafasi zao za kazi.

Aidha Mweli amesisitiza kuwa ili kufanikisha utendaji bora wa kazi lazima kila mtu ajipime katika utendaji kazi wake kwa kuhakikisha utendaji wake wa kazi unaleta matokeo chanya kwa taasisi na taifa kwa ujumla.

“Unapokuja kwangu na tatizo juu ya kukosoa njoo na suluhisho nini kifanyike ili kufikia malengo kwani adhima yetu ni moja ya kujenga taifa moja, hamna haja ya kuangalia nani kakosea” Amesema Mweli.

Mweli amewataka watendaji wake kuhakikisha wanakaa chini kwa pamoja na kutatua changamoto ya madeni ya walimu kama alivyo elekeza Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Magufuli kipindi anawaapisha Viongozi wapya Ikulu Jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

“Ili kutatua changamoto hii lazima sote kama watendaji tuvae uhusika wa majukumu yetu ili kuleta utendaji bora katika sekta ya elimu na kuboresha elimu nchini” Ameeleza Mweli

Naye Kaimu Mkurugenzi Idara ya Uratibu wa Elimu Dk. George Jidamva amezielezea Idara zilizopo chini ya Idara ya Elimu katika Ofisi ya Rais TAMISEMI na kuhainisha majukumu ya Sekta ya Elimu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Utumishi Ofisi ya Rais TAMISEMI Victor Kategere amesema kuwa watumishi wote wako tayari kushirikiana naye kwa hali na mali kuhakikisha wanaleta matokeo chanya katika utendaji kazi.

Ikumbukwe hivi karibuni kumefanyika uteuzi wa viongozi mbali mbali na Bwana Gerald Mweli anachukua nafasi ya Naibu Katibu Mkuu (ELIMU) TAMISEMI Bwana Mathias Kabunduguru aliyeteuliwa kuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania.

No comments:

Post a Comment

Adbox